Thursday, August 5, 2010

BREAKING Newwwwwwwwwwwws JIMBO LA KALENGA NI DK.MGIMWA NA SIYO KANDORO

Kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Iringa imetengua matokeo ya kura ya maoni jimbo la Kalenga yaliyompa ushindi Bwana Abas Kandoro na hivyo kumtangaza Dk.William Mgimwa kuwa ndiye mshindi wa kura za maoni katika Jimbo hilo.
Hatua ya kutengua matokeo hayo inafuatia Dk.Mgimwa kuilalamikia kamati hiyo kuhusu utata wa matokeo hayo yaliyompa ushindi Bwana Kandoro wakati hapo awali Dk.Mgimwa ndiye alikuwa ametangazwa kuwa mshindi.
Kufuatia hali hiyo kamati ya siasa chama cha mapinduzi iliketi kujadili uhalali wa matokeo haya na kubaini kuwa Kandoro hakuwa Mshindi wa kura za maoni katika Jimbo hilo.
Akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho,Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Iringa Bibi.Delfina Mtavilalo amesema baada ya kutokea kwa utata wa matokeo hayo kamati ililazimika kuwaita mawakala na kuwataka kuwasilisha kura zote zilizopigwa kwa kamati hiyo ili kubaini ukweli wa utata huo.
Amesema baada ya kupitia upya hesabu za kura na vielelezo mbalimbali imebainika kuwa Katibu kata wa CCM Ifunda Bwana Juma Habibu alichukua karibu kura 1212 za Dk.Mgimwa na kumuongezea kandoro na hivyo kumfanya aibuke na ushindi huo.
Alipoulizwa sababu za Katibu kata huyo kufanya kitendo hicho amesema amejitetea kuwa alichanganyikiwa na ndiyo maana alimpa Bwana Kandoro kura ambazo hakustahili.
Barua ya kubatilisha ushindi wa kandoro ambayo imesainiwa na Katibu wa CCM wilaya ya Iringa Bwana Luciano Mbosa imesema katika mchakato wa kura za maoni jimbo la Kalenga Dk.Mgimwa amepata kura 5212 dhidi ya kura 4200 za kandoro na kwa matokeo hayo inamtangaza Dk.Mgimwa kuwa mshindi na siyo Kandoro.

Baadhi ya wanachama wa CCM Jimbo la Kalenga wamemtuhumu Katibu wa CCM wilaya ya Iringa Bwana Luciano Mbosa kuwa ndiye chanzo cha kutokea kwa utata huo.

Wamesema Bwana Luciano wakishirikiana na Katibu kata wa Ifunda kwa maksudi walivuruga matokeo hayo baada ya kuahidiwa Nyumba na Fedha na Kandoro iwapo wangefanikisha kupitisha kuwa mgombea wa Ubunge katika Jimbo la Kalenga.

Hata hivyo inadaiwa kuwa mipango hiyo ilishindwa kufanikiwa kutokana na kutokuwa makini katika kuchanganya karata ambazo zingewezesha kumpa ushindi Bwana Kandoro.

No comments:

Post a Comment